Monday, October 29, 2012

Je unajua ni hatari kumdadisi mpenzi wako alitembea na wangapi?


KATIKA mapenzi kuna mambo ambayo hayastahili kupewa muda wa kuyajadili. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, mengine yanaweza kutibua furaha iliyopo na kuweza kupindisha maisha yenu.

Kwa kuthibitisha hilo, sikia kisa hiki. Jamaa mmoja aliyefahamika kwa jina la Rashid alibahatika kumpata mke mzuri sana aliyefahamika kwa jina la Wahida. Yaani mwanamke ambaye kila mwanaume akimuona ni lazima atamani kuwa naye.

Baada ya mwanaume huyo kumuoa, waliishi kwa muda mrefu sana na ndoa yao ilikuwa ikitawaliwa na furaha siku zote. Wakabahatika kupata watoto wawili. Hakika mwanamke huyo alikuwa mke kwa maana halisi ya mke.

Alikuwa akimheshimu sana mumewe na kumpatia kila aina ya furaha. Kwa kifupi ilikuwa ni ndoa ya kuigwa. Siku moja Rashid alikutana na rafiki yake wa muda mrefu sana.

Mazungumzo yao yalikuwa mengi lakini ikafika mahali yule rafiki akamuuliza Rashid kama ameshaoa. Rashid akajibu kuwa kamuoa msichana mmoja anayeitwa Wahida. Yule jamaa akashangaa kusikia Rashid kamuoa Wahida, mwanamke ambaye siku za nyuma alikuwa ni changudoa.

Rashid aliposikia kuwa Wahida alikuwa changudoa, ati akaumia sana na akaanza visa kwa mkewe na hatimaye wakaachana. Akaoa msichana mwingine dogodogo kutoka kijijini ambaye hajaguswa. Alichokiona kwenye ndoa yake hiyo ya pili alijuta hadi akamkumbuka Wahida.

Tunajifunza nini kwenye kisa hiki? Ni kwamba, unapokutana na mpenzi wako kwa mara ya kwanza kuna mambo ya msingi ambayo kiukweli unastahili kuyajua. Hapa namaanisha historia ya maisha yake. Unapotaka kujua historia ya maisha ya mpenzi wako siyo lazima kila kitu ujue. Mengine yaache abaki nayo kwani hata akikuambia hayawezi kukusaidia kiviiile.

Lipo hili swali la umeshwahi kutembea na wanaume/wanawake wangapi hadi leo? Hili si zuri kumuuliza mpenzi wako. Kwa nini nasema hivyo? Nina sababu mbili. Kwanza ni vigumu sana kupata jibu la kweli, yaani tarajia kudanganywa. Hapo unaweza hata kuambiwa hajawahi kuwa na mpenzi kumbe katika ukweli tangu ameyajua mapenzi, ametoka nao zaidi ya kumi.

Sababu nyingine ya kwa nini hustahili kuuliza swali hilo ni kwamba, inaweza kukufanya ukabadili mawazo yako na hata uhusiano wenu ukakomea hapo. Unaweza kukutana na msichana mzuri sana mwenye kila sifa nzuri na katika historia yake ya mapenzi anaweza kuwa ameshapita kwa wanaume kibao kiasi kwamba hata idadi amesahau.

Sasa kama utamuuliza na yeye akawa mkweli kwako kwa kukujibu kuwa, ni wengi kiasi kwamba hata idadi hakumbuki, utajisikiaje?

Hakika unaweza kujikuta unanyong’onyea na kushangaa hata ile hamu ya kuendelea kuwa naye inaisha licha ya kwamba hukustahili kuwa hivyo. Matokeo yake unaweza kumkosa mtu ambaye alistahili kuwa na wewe na mkaishi maisha ya raha mustarehe.

Kuwa na idadi kubwa ni tatizo?
Kuna mtaalam mmoja aliwahi kusema kuwa, katika maisha ya sasa hakuna mwanamke anayeolewa akiwa na usichana wake na kama wapo ni wachache sana. Akaeleza kuwa, msichana akishatolewa usichana wake hata akiwa ametembea na wanaume ishirini hana tofauti na yule aliyetembea na wawili tu.

Mtaalam huyo akasema, tena inawezekana aliyetembea na wengi akatulia kwenye ndoa yake kuliko yule aliyetembea na mmoja au hajaguswa kabisa. Hapo ndipo inapoonekana kwamba, kuwa na historia ya kwamba uliwahi kutoka kimapenzi na wanaume/wanawake wengi, hakuna madhara makubwa katika ndoa.

Ndiyo maana inashauriwa kulifutilia mbali swali la kutaka kujua idadi ya wapenzi aliyowahi kuwa nao huyo mpenzi wako au hata kuwajua kwa majina. Hii ni kwa sababu hata ukijua haitakusaidia chochote zaidi ya kukuchanganya na kukufanya ukose imani kwa mpenzi wako.

kama utakuwa umenufaika usiwe mchoyo mwambie na rafiki yako naye asome safu hii kupitia www.kishindoleo.blogspot.com

Makala hii kwa hisani ya mtandao wa Global Publishers

No comments: